Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika mwenye miaka 82 amejiuzulu. Bouteflika amejiuzulu baada ya miaka 20 ya utawala wake pamoja na maandamano makubwa yaliyodumu kwa wiki sita, yaliyolenga kumshinikiza kiongozi huyo kujiuzulu
Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika amejiuzulu. Bouteflika amejiuzulu usiku wa jana Jumanne(02.04.2019) baada ya miaka 20 ya utawala wake pamoja na maandamano makubwa yaliyodumu kwa wiki sita, yaliyolenga kumshinikiza kiongozi huyo pamoja na washirika wake wa karibu kujiuzulu.
Tangazo hilo la kujiuzulu limekuja muda mfupi baada ya mwito kutoka kwa mkuu wa jeshi na mwenye ushawishi mkubwa nchini humo la kumtaka Bouteflika ama kuachia madaraka au kutangazwa kikatiba kuwa hana uwezo tena wa kuongoza kutokana na udhaifu wa kiafya. Shamrashamra zilionekana kwenye maeneo mbalimbali mjini Algiers baada ya tangazo hilo huku polisi waliokuwa pembeni wakiwaangalia raia hao.
Baraza la katiba linatarajiwa kukutana hii leo kutangaza rasmi hatua hiyo. Kulingana na katiba, spika wa bunge anachukua madaraka kama rais wa mpito na baada ya siku 90 uchaguzi wa urais utaitishwa. Abdelkader Bensalah ndiye rais wa sasa wa bunge la Algeria, na mshirika wa karibu wa Bouteflika.
Bado haijawa wazi iwapo hatu ahiyo itatuliza hali ya mambo nchini humo, na hususan waandamanaji ambao pamoja na kumshinikiza Bouteflika kuachia ngazi, wanataka kufanyika kwa mageuzi katika mfumo mzima wa utawala unaohusisha washirika wake wa karibu.
Mwisho wa habari / 291